Jumanne 5 Mei 2026 - 10:59
Umoja wa mhimili wa muqawama na mshikamano wa vikosi vyake katika nyanja mbalimbali, leo umegeuka kuwa ukweli thabiti/ Taifa kubwa la Lebanon limetoa mfano wa kipekee wa ustahimilivu na uimara duniani.

Hawza/ Umoja wa mhimili wa muqawama na mshikamano wa vikosi vyake katika nyanja mbalimbali, leo umegeuka kuwa ukweli thabiti unaosimama juu ya irada yenye utambuzi na uongozi wenye hekima, na unaonesha muunganiko wa kina baina ya nguvu za taifa huru lililoshikamana na lengo moja: kulinda heshima na kusimama dhidi ya dhulma na uchokozi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, matini ya ujumbe wa Ayatullah A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza, kwa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Naim Qasim, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, ni kama ifuatavyo:

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن کُنتُم مُّؤْمِنِینَ

إِن یَنصُرْکُمُ اللَّهُ فَلَا غَالِبَ لَکُمْ

Mtukufu Allamah mpambanaji, Sheikh Naim Qasim; kiongozi wa muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon (Mwenyezi Mungu amlinde na amhifadhi),

Amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake.

Ninakuandikia kutoka moyoni mwangu; pale ambapo miale ya moto inawaka kwa nguvu na ngurumo za mizinga zinavuma kila upande; lakini juu ya kelele zote hizi, kuna sauti inayoinuka ambayo si radi inayoweza kuinyamazisha wala moshi wowote kuizima.

وَکَانَ حَقًّا عَلَیْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِینَ

Ahadi ya Mwenyezi Mungu kamwe haivunjwi, na mapambazuko ya ushindi, kadiri giza la uchokozi linavyozidi, ndivyo yanavyokaribia zaidi. Kambi ya muqawama, ambayo imesimama juu ya mantiki ya mbinguni na sunna zisizobadilika za Mwenyezi Mungu, inaendelea mbele kwa yakini na imani thabiti; kwa sababu inategemea nguzo isiyoweza kushindwa na inamtegemea Msaidizi ambaye hawaachi mawalii Wake.

Katika nafasi hii, kwa heshima na utukufu mkubwa, tunawakumbuka mashahidi waliopata shahada katika njia ya izza na heshima; na mbele yao, Imamu shahidi na kiongozi mwenye kuhamasisha, Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Khamenei, na pia shahidi mtukufu na kamanda wa kipekee wa kihistoria, Sayyid Hassan Nasrallah, ambaye basira yake ilikuwa taa ya njia ya mujahidina, maneno yake mwongozo wa muqawama, na damu yake takatifu ilikuwa ahadi mpya ya kudumu ya kuendelea kupeperusha bendera ya jihadi hadi kutimia kwa ahadi ya nusura ya Mwenyezi Mungu.

Ewe kamanda shujaa, wapiganaji wako mashujaa — watoto wa imani na kujitoa — waliamsha dhamiri ya dunia iliyokuwa imeelemewa na ukimya wa aibu na kulegea kutokana na misimamo dhaifu. Walichora kwa damu yao masomo ambayo historia haitayasahau kamwe, na kwa kujitolea kwao wakaumba visa vya kishujaa ambavyo vizazi vitavisimulia.

Vilevile, taifa kubwa la Lebanon, wanaume, wanawake na vijana wake wavumilivu, limetoa mfano wa kipekee wa ustahimilivu na uimara duniani, kiasi kwamba muqawama wake wa wananchi umekuwa alama ya izza na chanzo cha msukumo kwa mataifa yote yenye kiu ya uhuru na heshima. Ukuu wa muqawama huu haupo tu katika silaha zake, bali katika irada ya taifa hai lililoubeba na kushiriki nalo mzigo wa kujitoa muhanga.

Leo kusini si ardhi tu, bali ni moyo unaopiga kwa heshima na unaodunga heshima katika mishipa ya ubinadamu uliochoka. Hapo pamekuwa makaburi ya mizinga ambayo adui alikuwa akijivunia, na uwanja wa visa vya milele vilivyoandikwa na wana wa madrasah ya shahada.

کَم مِّن فِئَةٍ قَلِیلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً کَثِیرَةً بِإِذْنِ اللَّهِ

Mmeionesha dunia taswira angavu ya irada isiyoshindwa na taifa lenye uwezo wa kuvunja mitholojia za kijeshi na kufichua udhaifu wa mkoloni — hata kama mashine yake ya vita ni kubwa — na kubomoa nyumba yake ya buibui.

Aidha, umoja wa mhimili wa muqawama na mshikamano wa vikosi vyake katika nyanja mbalimbali leo umegeuka kuwa ukweli thabiti unaosimama juu ya irada yenye utambuzi na uongozi wenye hekima, na unaoonesha muunganiko wa kina kati ya nguvu za taifa huru lililokusanyika juu ya lengo moja: kulinda heshima na 

kusimama dhidi ya dhulma na uchokozi.

Watoto wa muqawama wamejitenga na mapambo ya kudanganya ya dunia, na kwa nyoyo zilizojaa imani na nafsi zenye shauku ya shahada, chini ya uongozi wenu wenye hekima na ujasiri, wamechukua njia ya kujitolea na kujitoa muhanga. Wamefungua milango ya mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa kila mtafutaji wa haki, na wakanywesha roho zenye kiu ya kukutana na Mola katika zama ambazo utupu wa kiroho na kuporomoka kwa maadili kumeongezeka.

مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ

Na cha kushangaza zaidi ni kwamba mshale wa muqawama haukukosea katika kumlenga adui wa kweli, na hii ni dalili wazi ya usafi wa basira ya vijana wake na hekima ya uongozi unaochora njia kwa uthabiti na upeo wa mbali.

Adui alikuwa ametegemea baadhi ya mapungufu ya ndani ili kuchochea fitna ya ndani na kuwasha moto miongoni mwenu, au kulazimisha vita vya pembeni ili kudhoofisha nguvu zenu na kuzitawanya. Lakini nyinyi — kama historia inavyowakumbuka — mlivuruga njama hii na kuigeuza hila yake kuwa kushindwa wazi na mipango yake yenye sumu kuwa majivu yaliyotawanywa.

Aidha, katika muktadha huu tunasisitiza kwamba; hawza, mara'ji' wa dini na idadi kubwa ya wanazuoni katika ulimwengu wa Kiislamu, wamesimama pamoja na muqawama huu uliobarikiwa na wanatangaza kuunga mkono kikamilifu, hususan kwa muqawama wa fahari wa Lebanon, na wako tayari kutumia kila aina ya msaada wa kiroho, kielimu na kivitendo kwa ajili ya kusaidia njia ya haki na uadilifu.

Bila shaka, ushindi ambao Mwenyezi Mungu amewaahidi mujahidina leo unaonekana kwa maana yake ya kweli kabisa. Bishara za ushindi huu zinajitokeza kwa kila wakati wa ustahimilivu na kwa kila msimamo unaothibitisha kuwa haki itashinda hata kama muda utachelewa, na batili ni ya kuangamia hata kama sauti yake ni kubwa.

وَیَوْمَئِذٍ یَفْرَحُ الْمُؤْمِنُونَ * بِنَصْرِ اللَّهِ

Tunakupongeza kwa ustahimilivu huu wenye baraka, na tunatangaza kuwaunga mkono kwa nguvu zote, na tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupeni daima tawfiki na uthabiti, na kwa mikono yenu autimize ushindi kamili na kuondoka kwa ukaliaji, na akufanyeni kuwa chanzo cha kheri na kinga dhidi ya shari.

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ إِنَّ الْبَاطِلَ کَانَ زَهُوقًا

Na amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake.

وَاللَّهُ غَالِبٌ عَلَی أَمْرِهِ وَلَکِنَّ أَکْثَرَ النَّاسِ لَا یَعْلَمُونَ

Ali Reza A‘rafi
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha